1.0 UTANGULIZI
1.1. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusimamia shughuli za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini. Kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni za EPOCA (CEIR) za mwaka 2011 zimewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
1.2. Mfumo huu wa kielektroniki ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Desemba 2015 na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi (IMEI) kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano. Namba tambulishi za vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo kesho tarehe 16 Juni 2016.
1.3. Kipindi cha mpito cha kuelimisha umma pamoja na zoezi la wateja kuhakiki simu walizo nazo au wakati wanataka kununua simu mpya lilianza mwezi Desemba 2015 wakati mfumo ulipozinduliwa na litamalizika kesho tarehe 16 Juni 2016. Hata hivyo, elimu kwa umma kuhusu simu bandia imekuwa ikitolewa nchini tangu mwezi Novemba 2011 baada ya Kanuni za CEIR kutoka, kufuatia kupitishwa na Bunge Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta tarehe 20 Juni 2010 ikielekeza kuwekwa kwa mfumo wa namba za utambulisho wa vifaa vya Mawasiliano vya kiganjani.
2.0 KAZI ZILIZOFANYIKA TANGU KUZINDULIWA KWA MFUMO
2.1 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea kusimamia kwa karibu makampuni ya simu hapa nchini katika uendeshaji wa kila siku wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Hii imesaidia pamoja na mambo mengine kupata taarifa za namba tambulishi (IMEI) na kuzifanyia uchambuzi wa kina ili kupata mwelekeo halisi kabla ya kipindi cha mpito kuisha hapo tarehe 16 Juni, 2016.
2.2 Mamlaka ya Mawasiliano iliendelea pia na kampeni za kutoa elimu kwa umma kuhusu jinsi ya kuhakiki namba tambulishi (IMEI) za vifaa vya mkononi (mobile devices). Katika kampeni hizo wananchi walipata uelewa wa kutambua uhalisia wa simu zao ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu mpya. Makampuni yote ya simu hapa nchini kwa nyakati tofauti wameshiriki pia katika kuelimisha umma, ikiwa ni pamoja na kuwapelekea ujumbe mahususi moja kwa moja kwa watumiaji wote wa simu za mkononi. Hali kadhalika Shirika la Viwango Tanzania na Tume ya Ushindani nchini, wameshiriki moja kwa moja katika kutoa elimu kwa umma sambamba na Mamlaka ya Mawasiliano.
2.3 Kipindi cha kuanzia Desemba 2015 mpaka mwezi Mei 2016 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa elimu kwa umma katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Dodoma, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera. Pia elimu kwa umma ilitolewa Zanzibar. Mamlaka imefanya pia elimu kwa umma katika miji ya, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara wiki iliyopita pamoja na wiki hii. Aidha kesho ambayo ndio siku ya ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini, kutakua na mkutano wa wafanya biashara wa simu wa mkoa wa Dar es Salaam. Mkutano huo utawahusisha pia mafundi wa simu, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa. Pamoja na mikutano ya hadhara na mikutano ya barabarani (road shows), elimu imetolewa kwa wauzaji wa simu, Mafundi wa Simu na Maafisa Biashara pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo husika.
3.0 UCHAMBUZI WA NAMBA TAMBULISHI (IMEI)
Wakati mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi unazinduliwa mwezi Desemba 2015, idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilikuwa sawa na 4% na zile ambazo zilikuwa zimenakiliwa (duplicates) zilikuwa ni sawa na 30%. Hii ikiwa na maana 66% ni sio simu bandia. Uchambuzi huu haukuhusisha taarifa za makampuni ya Viettel na Smile.
Uchambuzi wa mwezi Februari 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 18%. Simu halisi zilikuwa sawa na 79%.
Uchambuzi wa mwezi Machi 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 13%. 83% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu nchini.
Uchambuzi wa mwezi Aprili 2016 unaonyesha hakuna mabadiliko yoyote ya idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) hivyo kubakia 4%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa ziliongezeka kutoka 13% na kufikia 14%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia ilipungua kutoka 83% mpaka 82% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo kifuatacho.
Matokeo ya uchambuzi wa mwezi Aprili, 2016 umeonyesha namba tambulishi ambazo zilikua zimenakiliwa kuongezeka na kuleta taswira kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa wauzaji wa simu wasio waaminifu kupunguza bei za simu zao zenye namba tambulishi zilizonakiliwa na kuwafanya watumiaji wa simu katika maeneo husika ambayo elimu kwa umma ilikua bado haijawafikia kushawishika kununua simu hizo. Matokeo haya yalitoa msukumo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na wadau wote kuongeza nguvu zaidi kuelimisha wananchi katika maeneo yaliyobakia kuhusu umuhimu wa kuhakiki simu zao ikiwa ni pamoja na kuelewa zaidi utaratibu wa kufuata wakati mtu atakapo hitaji kununua simu mpya.
Uchambuzi wa mwezi Mei, 2016 ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na 3%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na 2% ambapo 95% zikiwa simu halisi. Uchambuzi huu unahusisha taarifa za makampuni yote ya simu nchini.
Matokeo haya mazuri yanaonyesha matokeo ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Makampuni ya simu hapa nchini pamoja na wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya kuhakiki uhalisia wa simu walizo nazo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu mpya.
Uchambuzi uliofanywa tarehe 14 Juni 2016 unaonyesha mabadiliko chanya ya idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (invalid) kupungua kutoka 3% hadi kufikia 2.96%, na idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zikipungua kutoka 2% hadi kufikia 0.09%. Vilevile idadi ya namba tambulishi za simu halisia zimeongezeka kutoka 85% mpaka 96.95% kama ilivyoonyeshwa katika kielelezo 6 hapo juu.
Matokea haya yanaonyesha mwitikio mzuri wa wananchi juu ya uelewa wao katika suala zima la uzimaji wa simu ambazo hazikidhi viwango. Matokeo hayo yanatoa picha nzuri hasa tunapoelekea kuhitimisha zoezi la uzimaji wa simu bandia kesho tarehe 16 Juni 2016.
4.0 CHANGAMOTO
Pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wengine bado kuna changamoto ambazo zinahitajika kutatuliwa. Changamoto hizo ni pamoja na:
(i) Uaminifu mdogo kwa baadhi waauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu;
(ii) Gharama zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na kuelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu zao; na
(iii) Uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi katika kuitikia wito wa kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito.
5.0 HITIMISHO
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaendelea kumbusha watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio bandia kwani kuanzia kesho, hakuna simu bandia itakayoweza kufanya kazi nchini. Vilevile Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kutambua kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi (mobile devices) kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka kumi (10) au faini isiyopungua TZS millioni 30 au vyote kwa pamoja.
Mamlaka inatoa wito kwa wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu hapa nchini kutoka nje wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa mujibu wa Shirika la Viwango Tanzania. Aidha Mamlaka inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa mafundi wote wa simu nchini, wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inayapongeza makampuni ya simu kwa ushirikiano mzuri wanaondelea kuuonesha katika kutekeleza agizo hili la Serikali kupitia Mamlaka. Hali kadhalika, jitihada zao za kushiriki elimu kwa umma kwa wateja wao pamoja na kuwapatia simu wateja waliokuwa wanatumia simu bandia, kumepelekea agizo hili kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu. Mafanikio ya jambo hili, kwa kiasi kikubwa yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa Mawasiliano, wakiwemo jeshi la Polisi, Tume ya Ushindani pamoja na Shirika la Viwango Tanzania.
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani. Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia garantiii ya miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika, taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki ya simu husika.
2. Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu. Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu iliyopotea (risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo).
Mtoa huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani ya saa 24.
3. Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.
No comments:
Post a Comment