Friday, 29 April 2016

NWANKWO KANU AMUONGELEA MBWANA SAMATTA, AMPA MBINU ZA KUMFANYA AFIKE MBALI ZAIDI.

GWIJI wa soka wa zamani wa timu ya Taifa ya Nigeria `Super Eagles’ na klabu ya Arsenal ya England, Nwankwo Kanu amesema kwa sasa soka la Tanzania linajulikana baada ya mchezaji, Mbwana Samatta kusajiliwa na Klabu ya KRC Genk inayoshiri Ligi Kuu Ubelgiji.
Mbali ya Arsenal, nyota huyo amecheza pia klabu za West Brom na Portsmouth za England, Inter Milan ya Italia na Ajax Amsterdam ya Uholanzi aliyoisaidia kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu wa 1994/95 akiwa kinda wa miaka 19 tu.
Kwa sasa Kanu ana umri wa miaka 39. Pia Kanu amesema ili soka la Tanzania liweze kukua na kuwa na wachezaji wengi zaidi watakaoweza kucheza soka la kulipwa barani Ulaya ni lazima izingatiwe uanzishwaji wa vituo vingi vya kulelea vipaji vya vijana.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akizindua duka jipya la Startimes lililopo katika Jengo la Mkuki, Kanu alisema awali alikuwa akilijua soka la Tanzania kwa kupitia timu ya taifa pale ilipokuwa inacheza mechi za kimataifa za kirafiki au za mashindano.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania, nimekuwa Kenya na Uganda, na nilikuwa nalijua soka la Tanzania kupitia timu ya taifa, lakini kwa sasa nalijua baada ya Mbwana Samatta kusajiliwa na Genk,” alisema Kanu.

Alisema ili Tanzania iwe na akina Samatta wengi katika soka la kulipwa Ulaya, inatakiwa kufanya jitihada za makusudi za kujenga msingi mzuri wa kukuza wachezaji vijana. “Naamini kama Tanzania itakuwa na vituo vingi vya kulelea vipaji vya wachezaji vijana, mtaweza kuwa na wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya kama ilivyo kwetu Nigeria,” alisema.
Kanu alisema kuwa katika kupata wachezaji wengi hakuna njia ya mkato, ni lazima nchi ijitahidi kuzalisha na kukuza vipaji vingi vya wachezaji kama ilivyo katika nchi za Afrika Magharibi.
Kanu yupo nchini kwa ziara ya siku nne ukiwa ni mwaliko wa Startimes ambayo ni balozi wake na kesho atakuwa Mbagala Zakhem, ambako atakutana na wachezaji wadogo wa soka. Mbagala ni eneo alikokulia Samatta.

NAIBU SPIKA TULIA ACKSON, AMWITA MBUNGE WA CUF "BWEGE"..

 

Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo. 

Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”. 

Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege. 

Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.” 

Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika. 

Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini. 

“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali. 

Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika. 

“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,” alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati. 

Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba? Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?

Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.

Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege. 

Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu. 

Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa viti maalumu (Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na kumponda Nape na uamuzi wa Serikali. 

Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa. 

“Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape vuvuzela,” alisema. 

“Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa moja?” 

Wakizungumzia tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge. 

“Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji. 

Alisema mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria. 

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.” 

Alisema Bunge linapaswa kuongozwa kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo inawafanya wabunge wa CCM waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani. 

“Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema. 

Kwa takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa vyama vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi ya Rais na kurejesha uhai kwenye chombo hicho. 

Katika hoja zao jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu ya Tano kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa kusitisha matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa mara kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni za Bunge. 

Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa ufafanuzi wao, walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa maelezo kuwa ndiye aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo. 

Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala bora na unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala bora. 

“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana nzima ya utawala bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa ufanisi, tija na kwa uwazi, uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa watu kwa kufuata utawala wa sheria,” alisema. 

Alisema ni ajabu Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni wakati nchi haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali. 

“Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji Msigwa. 

Alisema licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai kuwa hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na kuukosoa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli. 

“Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija bungeni mnakaa kimya.Huwa tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja humu ndani,“ alisema Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa ni mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama kuomba mwongozo, kupinga kauli ya mbunge huyo. 

Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68 (7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka Mchungaji Msigwa athibitishe kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri wanaopingana na uongozi wa Serikali. 

Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha 63 (1) (2), kinachomtaka mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo ama apewe muda na kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na Mchungaji Msigwa kuwasilisha ushahidi wao. 

Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia? Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge. 

Msigwa: Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio mwongozo ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa. Ila tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba. 

Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana. 

Akiendelea na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja. 

“Bunge ni mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza kuminya na kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya fedha za Watanzania,” alisema. 

“Serikali inayokandamiza uwazi ni Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu. Mnasimama na kusema mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha nini kuwaonyesha Watanzania hiki mnachokifanya?” 

Huku akiipongeza Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii watu kuzungumza na kusema ukweli. 

“Nyinyi mmekuja na ‘hapa kazi tu’, lakini hamtaki kukosolewa. Wakati tunamkosoa Kikwete wabunge wa CCM mlikaa kimya na kutuzomea, leo mnaufyata na inaonekana hata Dk Magufuli akidondosha kijiko, mtasimama na kupiga makofi kwa sababu ya uoga wenu,” alisema Mchungaji Msigwa na kuwataka wabunge kuhoji mambo kwa maslahi ya wananchi.

MAMA DIAMOND AMFYATUKIA ZARI THE BOSS LADY,AFICHUA SABABU ZA KUM DELETE


Muziki wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akiwa na mwandani wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady.
Kimenuka tena! Hali ndani ya familia ya staa wa Muziki wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, inadaiwa kuwa si shwari kufuatia mama wa msanii huyo, Sanura Kassim ‘Sandra’ akishirikiana na mwanaye Esma Platnumz kudaiwa kutibuana na mwandani wa jamaa huyo, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ Ijumaa lina ubuyu kamili.Chanzo cha kuaminika kilichoomba hifadhi ya jina kilidai kuwa, sababu ya kutibuana huko ni baada ya Zari kunasa umbeya kuwa, Esma amemkuwadia Diamond kwa yule video queen aitwaye Irene au Lynn kisha mama Diamond kumkumbatia mrembo huyo na kudai ni mwanaye.


BOFYA HAPA KUSIKIA CHANZO
“Ukweli ni kwamba hali si shwari ndani ya familia ya Dangote (Diamond), Zari amemaindi sana kusikia Esma kamuunganishia Diamond kwa yule Lynn (aliyeuza nyago kwenye video ya msanii wa Diamond aitwaye Raymond inayokwenda kwa jina la Kwetu), halafu na mama yake naye anamkumbatia.
“Kitendo kile kilimfanya Zari ajione kuwa hatakiwi. Kimsingi kilinuka na hata wakati Zari anaondoka kwenda South (Afrika Kusini), hali haikuwa poa.
MTANDAONI NAKO
Inaelezwa kuwa, kufuatia kutibuana huko, hivi karibuni Zari alimuunfollow (kumtoa kwenye listi ya watu wake) Esma kwenye akaunti yake ya Mtandao wa Instagram, jambo
lililoshibisha yale madai kuwa ni kweli kimenuka.
Aidha, ilidaiwa pia kuwa, kutokana na figisu hizo, Mama Diamond naye aliamua kufuta picha zote za Zari kwenye akaunti yake ya Instagram kuonesha kuwa amemchoka. “Wewe fuatilia huko Insta utaelewa hiki ambacho nakuambia, kwa kifupi ni kwamba Zari, Esma na mama yake ni mvurugano,” kilisisitiza chanzo hicho ambacho kiko karibu na familia hiyo.
HUYU HAPA MAMA D
Kufuatia madai hayo, Ijumaa lilifanya jitihada za kumsaka mama Diamond kuzungumzia madai hayo ambapo alipopatikana alimfyatukia Zari kwenye mahojiano ya dakika 45 huku akianika kilicho nyuma ya pazia;
Ijumaa: Kuna madai kuwa wewe na Zari mmetibuana na kutokana na hilo umefikia hadi hatua ya kufuta picha zake Insta, hilo likoje mama? Mama Diamond: Hayo mambo ya kutibuana yapo tu, siyo kwetu hata kwenye familia nyingine. Ninachojua sasa hivi tuko sawa ila hilo la kufuta picha liko hivi; nimefanya hivyo kwa kuwa nataka nitoke kwenye Insta na sijafuta za Zari tu, nimefuta zote na kubakiza za wajukuu, ya Diamond na Rommy Jones.
Ijumaa: Inadaiwa hali si shwari kwenye familia baada ya Diamond kudaiwa kutoka na msichana aitwaye Lynn, mama unasemaje kuhusu hilo? Mama Diamond: Haya matimu kwenye mitandao ndiyo yanazusha mambo ya ajabu, mbona mambo mengine ni ya kawaida kutokea.
Mimi ni mama hapa nyumbani, hivyo siwezi kumtafutia Diamond mwanamke wala mtu yeyote na msimamo wangu mimi kila aliye kwenye himaya yangu kwangu ni mtoto siwezi kumbagua.
Swali: Inadaiwa Zari anakuchukia kwa sababu umemkumbatia Lynn na kusema ni mwanao wakati anahisi anatoka na Diamond, hili likoje? Mama Diamond: Sina ugomvi na mtu ila Zari akinichukia, ananichukia mwenyewe, mimi sina tatizo, ujue mimi ni mama maana hata mtu akija kuniuliza eti fulani ana mwanamke nakuwa sijui lolote.
ESMA NAYE ANENA Kufuatia madai ya kutibuana, Esma naye alipotafutwa alikuwa na haya ya kunena: “Kwenye maisha ya siku zote watu kugombana ni jambo la kawaida. Hata hivyo, nimekuwa nikisikia mara kadhaa watu wakinituhumu kuwa namkuwadia Diamond, mara nimegombana na Zari, hayo ni maneno ya watu tu yanayozushwa kwenye mitandao.
“Suala la kusema mimi huwa namkuwadia wanawake Diamond, kwanza watu watakuwa wananikosea adabu sana maana Diamond ni mtu mzima na ana maamuzi yake hivyo mimi siwezi kumtafutia demu. “Hilo la kwamba Zari ameni-unfolow kwenye Insta mimi sijui.”
TUJIKUMBUSHE Mara kwa mara kumekuwa na mvurugano kati ya Zari na mama Diamond akishirikiana na Esma huku utofauti za kimaisha kati Zari aliyezaa mtoto mmoja na Diamond, Latiffah Nasibu ‘Princes Tiffah’ kwani kumekuwa na madai kwamba mama Tiffah amekuwa akitaka kuleta uzungu.
Mbali na hilo, hivi karibuni kuliibuka madai kwamba, Lynn amekuwa akikumbatiwa na mama Diamond na Esma huku wakidaiwa kujua kuwa ni mchepuko wa Diamond, jambo linalozidi kuchochea fukuto kwenye familia hiyo ambapo Zari anadaiwa kujichimbia Sauz (Afrika Kusini).

Thursday, 28 April 2016

MAJAMBAZI MATATU YAUWAWA - CHUNYA, YALITAKA KUVAMIA DUKA LA VINYWAJI

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya  Butusyo Mwambelo akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya  (Hawapo pichani)katika kuzungumzia tukio la kuuwawa kwa majambazi watatu wakati wakijaribu kufanya uhalifu katika duka la kuuzia  vinywaji mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha silaha aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine ambayo ilikuwa ikitumika na majambazi hao katika tukio la kutaka kufanya uhalifu kwenye duka la vinywaji mali ya Hamisi mji mdogo wa Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya April 27 mwaka huu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo akionyesha silahaaina ya panga ambalo linadaiwa kutumiwa na majambazi hao .
Baadhi ya askari polisi wakifuatilia kwa makini mkutano wa kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa mbeya Butusyo Mwambelo wakati akizungumza na waandsihi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa majambazi watatu waliotaka kufanya uhalifu katika duka la vinywaji vya jumla linalomilikiwa na ndugu Hamisi Mkazi wa Matundasi Chunya Mkoani Mbeya .
Silaha mbalimbali zilizo kamatwa katika tukio la kuuwawa kwa majambazi wilayani Chunya mkoani mbeya April27 mwaka huu.
Na EmanuelMadafa,(Jamiimojablogu-Mbeya)
JESHI  la Polisi mkoani Mbeya  limewauwa watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wa kurushiana rasasi.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Butusyo Mwambelo amesema tukio hilo limetokea April 27 mwaka huu saa 2 usiku , huko katika kijiji cha Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya .
Amesema watu watano  wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na bunduki moja ya aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 na risasi 26 kwenye magazine , walifika kijijini hapo  kwa lengo la kufanya uhalifu kwenye duka la jumla la kuuzia vinywaji  mali ya Ndugu Hamis Mkazi wa eneo hilo la Matundasi Chunya..
Kamanda Mwambelo , amesema watu hao ambao miili yao imehifadhi kwenye chumba cha mochwari katika  hospitali ya wilaya ya Chunya , majina na makazi yao bado hayajajulikana.
Akifafanua, amesema taarifa za siri kutoka kwa raia wema zilifikia jeshi la polisi na ndipo askari polisi walipofika kwenye eneo la tukio.
“Baada ya polisi kufika katika eneo la tukio  watu hao walistuka kuwa wanafuatilwa na askari polisi na hivyo kuanza kukimbia kuelekea kijiji cha Matondo  kwa kutumia pikipiki yenye namba za usajili MC 761. AFS   aina ya Sanlag yenye rangi nyeusi”,amesema Mwambelo .
Amesema walipoona Polisi wanawakaribia walianza  kurusha  risasi hovyo hewani ambapo jambazi mmoja alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi mguuni na tumboni na kufariki dunia ambapo majambazi wanne walifanikiwa kutoroka .
Amesema kutokana na hali hiyo jeshi hilo la polisi lilianzisha msako usiku huo   na kufanikiwa kuwaua majambazi  wengine wawili  ambao huku wengine wakitoroka ambapo msako mkali unaendelea ili kuwakamata wahalifu hao.
Amesema katika eneo la tukio, ilipatikana
bunduki moja aina ya SMG yenye namba 1996 AFU 1120 ikiwa na risasi 27  kwenye magazine.  Pia pikipiki iliyokuwa iantumiwa na majambazi hayo, iliwezea kupatikana pamoja na panga .
Mwambelo  alitoa wito kwamba wananchi waendelee na moyo huo huo wa kuwafichua watu wanaowatilia shaka ili waweze kudhibitiwa mapema kabla ya kufanya uhalifu sanjali na kufika katika hospital ya wilaya ya Chunya kwa lengo la kufanya utambuzi wa miili ya majambazi hao kwani majina yao bado hayajatambulika.