Thursday, 14 April 2016
Mahakama ya Kisutu, yamwachia huru William Mhando wa TANESCO, Mkewe na Wenzao
BOSI TANESCO HURU: Korti ya Kisutu yamwachia huru aliyekuwa mkurugenzi wa Tanesco William Mhando na wenzake walioshtakiwa naye kwa matumizi mabaya ya Madaraka kwa kukosa ushahidi.
William Mhando, mke wake Eva Mhando, na wenzao watatu, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam tarehe 27,May 2014, wakikabiliwa na mashitaka sita ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kujipatia Sh. Milioni 31.7 kwa njia ya udanganyifu.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai alidai kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco jijini Dar es Salaam, Mhando akiwa mwajiriwa kama Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia vibaya mdaraka yake.
Alidai kuwa, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kwa kuangalia maslahi yake binafsi baada ya kuipa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kampuni hiyo inayongozwa na mke wake, Eva na watoto wake, vyenye thamani ya Sh. Milioni 884.5 na kuisababishia kampuni hiyo kupata faida ya Sh. 31,747,000 kinyume cha sheria .
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 6 na Julai 30, mwaka 2011, mahali pasipofahamika, jijini Dar es Salaam, Eva alighushi taarifa ya ukaguzi wa fedha ya Kampuni ya Santa Clara Ltd, akionyesha kwamba imekaguliwa na Finx Capital House Desemba mwaka 2010.
Swai alidai katika shitaka la tatu, Agosti 9, mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Eva alighushi nyaraka za umiliki wa hisa kutoka Santa Clara Supplies Ltd kwenda Eveta John Shing’oma huku akijua siyo kweli.
Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la nne, Agosti 5, mwaka 2011 katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, jijini, mshtakiwa Eva aliwasilisha nyaraka za manunuzi za kughushi akionyesha kwamba taarifa hiyo imeandaliwa na Finx Capital House huku akijua siyo kweli.
Katika shitaka la tano, ilidaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Oktoba 31, mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, Eva akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Santa Clara Limited kwa nia ovu, alijipatia faida ya Sh. Milioni 31.7 kutoka Tanesco baada ya kuwasilisha nyaraka za ukaguzi za kughushi.
Ilidaiwa katika shitaka la sita, Oktoba 17, mwaka 2011 katika ofisi za Tanesco, mshtakiwa wa tatu hadi wa tano, Mchalange, Misidai na Kisinga wakiwa watumishi wa shirika hilo, walipokea nyaraka za kughushi na kusababisha Kampuni ya Santa Clara Supplies Limited kupewa mkataba wa kusambaza vifaa vya ofisini.
Ilidaiwa kuwa mkataba huo ulisababisha kampuni hiyo kupata mkataba wa zabuni ya kusambaza vifaa vya Sh. Milioni 884.5 na kupata faida ya Sh. Milioni 31.5.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment