Monday, 11 April 2016
UNDANI WA KIFO CHA NDANDA KOSOVO,MENGI YAELEZWA
Msiba! Tasnia ya Muziki wa Dansi Bongo imegubikwa na simanzi nzito kufuatia kifo cha aliyewahi kutikisa vilivyo kwa rap na vibao vikali, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ndanda Kosovo ‘Kichaa’ aliyefikwa na umauti wikiendi iliyopita, Wikienda limechimba undani wa habari hiyo.
Habari zilizolifikia Wikienda mara tu baada ya kutokea kwa msiba huo asubuhi ya Jumamosi iliyopita zilieleza kuwa, Ndanda alisumbuliwa na tumbo ambapo alilazwa kwenye Hospitali ya Mwananyama na baadaye kuhamishiwa Muhimbili jijini Dar.
Akizungumza na Wikienda, mjomba wa Ndanda ambaye pia ni mwanamuziki, Cardinal Gento alisema kuwa, Ndanda alihamishiwa Muhimbili baada ya tatizo lake kushindikana Mwananyamala.
“Nilikesha naye hospitalini, ilipofika asubuhi nikaondoka kurudi nyumbani kwa ajili ya chakula, nikaacha anafanyiwa mpango wa damu maana alikuwa amepungukiwa, lakini muda mfupi baada ya kuondoka, nikapigiwa simu amefariki dunia,” alisema Gento wakiendelea na utaratibu wa msiba nyumbani kwa Ndanda, Madale, Dar.
Kabla ya kukutwa na umauti, historia ya ugonjwa wake inaonesha ilianza mwaka jana ambapo aliripotiwa na Magazeti ya Global kuwa alilazwa kwenye Hospitali ya PKA iliyoko Tegeta, Dar akisumbuliwa na tatizo la kupasuka kwa mmoja wa mishipa tumboni hivyo kutapika damu.
HISTORIA FUPI YA NDANDA KOSOVO
Ndanda aliwika na Bendi ya FM Academia International ambapo alitunga nyimbo za FM Academia baada ya kutoka jela akiwa na akina Nyoshi El-Sadaat, Maluu Stonch, Mulemule FBI, King Blaize, Patcho Mwamba, Gento na wengine kibao waliotamba na Wimbo wa Wajelajela.
Baadaye Ndanda alitoka FM Academia International akaanzisha Bendi ya Stono Musica akiita Wajelajela Original akiwa na Maluu, Chai Jaba, Patcho na wengine. Miongoni mwa nyimbo zake zilizotamba ni pamoja na Binadamu pamoja na rap zake za Kidedea na Kaokota Big G.
Baadaye Ndanda aliachana na Stono Musica akaelekea Marekani kwa shughuli za kimuziki ambazo zilikuwa na mafaniko makubwa. Aliporejea Bongo ndipo akaanzisha Kundi la Watoto wa Tembo kabla ya kuachana na bendi na vikundi na kuwa msanii anayejitegemea. Stori: Musa Mateja na Sifael Paul, Wikienda
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment