Kiongozi huyo amesema anaushahidi wa moja kwa moja juu ya vitendo vinavyofanywa na Waziri huyo katika kueneza propaganda zinazolenga kuiyumbisha Serikali .
“Nina ushahidi usio na mashaka wa Kitwanga kupanga Vijana wanaojiita wa UVCCM kufanya mikutano na Waandishi wa Habari na anawalipa fedha kufanya hivyo, nataka ieleweke wazi kuwa nina muunga mkono Rais katika kazi ya kusafisha Nchi … nitakuwa mtu wa ajabu nisipo muunga mkono katika vita dhidi ya ufisadi” amesema Zitto Kabwe.
Zitto amemtaka Waziri Kitwanga kuepuka siasa za porojo na kusema waziri huyo si ‘size’ yake na hana mpango wa kumtoa katika nafasi ya uwaziri hivyo aache kulalamika na kueneza uzushi.
“Kimsingi nashangaa mtu kama yeye (Kitwanga) kuweza hata kuwa Waziri wa Wizara nyeti kama hiyo, zaidi ya yote Waziri Kitwanga sio ‘size yangu’. Naanzaje kuhangaika na Kitwanga? Ili iweje? Namsihi asijipandishe chati kwamba mimi nataka kumtoa (uwaziri) . Ningetaka kumtoa wala asingejua maana ningeshughulika na aliyemteua” Amesisitiza Kabwe.
Hata hivyo Kabwe amemtaka Waziri Kitwanga kujipima kama bado anastahili kuendelea kukaa katika nafasi yake ya uwaziri kutokana na kashfa ya kampuni anayo imiliki iitwayo Infosys kwa kushirikiana na Kampuni ya Lugumi kuiingizia Serikali hasara ya shilingi bilioni 34 kupitia Zabuni ya kununua vifaa vya kutekeleza mradi wa utambuzi wa vidole kwenye Vituo vya Polisi nchini.
“Nawasihi Watanzania wote kumdharau Waziri Kitwanga nakumtaka ajibu tuhuma zinazomkabili za kampuni yake binafsi kufanya kazi na Idara katika Wizara anayosimamia na kwamba ajipime kama anatosha kuendelea kumsaidia Rais kazi.” Aliongeza Kabwe
No comments:
Post a Comment