Monday, 25 April 2016

HII NDIO HISTORIA YA MAREHEMU PAPA WEMBA

Image copyrightCourtesy
Image captionMarehemu Papa Wemba
Habari kuwa mmoja wa vigogo wa muziki wa kiafrika Papa Wemba ametutangulia mbele ya haki imepokewa kwa mshtuko mkubwa na mashabiki wake kote duniani.
Video inayosambazwa katika mitandao ya kijamii inamuonesha Papa Wemba akiendelea na kazi yake anayoifahamu zaidi ya uimbaji kisha anaonekana akianguka ghafla jukwaani.
Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba 1949-2016.
Wanabendi wake waliokuwa jukwaani naye huko Abidjan katika tamasha la muziki la #FEMUA wanaendelea kupiga densi tu kabla ya mmoja wao kukimbia kumuokoa baada ya kuona kasalia chini kwa sekunde kadhaa akiwa anatetemeka kisha akazirai.
Shoo hiyo ya Papa Wemba ilikuwa moja katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan.
Msemaji wake Henry Christmas Mbuta Vokia, ameiambia Radio Okapi kuwa
''Marehemu Papa Wemba alikuwa ameingia muda mchache tu jukwaani kisha akacheza wimbo wa kwanza, mashabiki wakamuomba awaimbie tena wimbo mwengine akakubali.
lakini dakika chache tu baada ya kuanza kupiga wimbo wake wa tatu Papa Wemba alianguka na kuzirai ghafla jukwaani''
Watu wa shirika la msalaba mwekundu walijaribu kumsaidia lakini hakuonesha dalili nzuri kwa hivyo wakampeleka hospitalini kwa dharura lakini baada ya dakika karibu thelathini hivi tukaambiwa kuwa Papa Wemba ametuacha''
Alisema Mbuta Vokia.
Msanii huyo nguli alikonga nyoyo za wapenzi wa muziki wa Soukus nchini DRC na kote duniani kwa kipaji chake cha kipekee na sauti isiyokuwa na mfano.
Wengi waliitambua sauti hiyo ya na utunzi wake.
Alikuwa ni mtumbuizaji kamili.
Ni mweledi wa kuimba kucheza ala za muziki na pia kusakata rhumba yaani kunengua kiuno.
Lakini je Papa wemba ni nani ?
Gwiji huyo wa muziki wa lingala alizaliwa mnamo Juni 14 mwaka 1949, katika eneo la Lubefu - Wilaya ya Sankuru nchini Congo.
Jina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba.
Yeye alianza kazi ya muziki akiwa na umri mdogo mno.
Alikuwa akimfuata mamake katika matanga na hivyo akaibukia kuwa mtunzi wa nyimbo za kuomboleza.
Alitunga wimbo wake wa kwanza "Madrigal" akiwa na umri wa miaka
Shungu Wembadio alijiunga na kundi la ''Stukas'' kabla ya kuliacha na kuunda kundi kubwa la Zaiko langalanga mwaka huohuo wa 1969.
Zaiko Langalanga Sauti yake ya kipekee na uweledi wake uliisaidia kundi hilo katika utunzi wa "Pauline", "Chouchouna", "Liwa is somo".
Wemba wakati huo alijiunga na wanamuziki wenza wa Zaire (Congo ilivyojulikana wakati huo) Nyoka Longo Jossart, Manuaku Pepe Felly, Evoloko Lay Lay, Bimi Ombale, Teddy Sukami, Zamuangana Enock, Mavuela Simeon, Clan Petrole miongoni mwa wengine.
Wakati huo akianza Papa Wemba , jukwaaa la muziki nchini humo lilikuwa limetawalwa na vigogo wa muziki Franco Luambo wa TPOK Jazz, Tabu Ley Rochereau wa Afrisa, na makundi mengine mapya kama vile Les Grands Maquisards, Le Trio Madjesi, Bella-Bella, Thu Zaina na Empire Bakuba.
Hata hivyo sauti ya kipekee ya Papa Wemba akijulikana wakati huo kwa majina yake kamili Jules Presley Shungu Wembadio ilikonga mioyo ya wapenzi wa Soukus.
Kilele cha ufanisi wa kundi la Zaiko Langa Langa ulikuja miaka ya mapema ya sabini.(1973)
Hapo ndipo Shungu alibadili jina lake na kuanza kuitwa jina la utani ''Papa Wemba''.
Yolele
Miaka mitano baadaye aliihama kundi hilo na kujiunga na "Isifi Lokole" hapo alitunga wimbo maarufu wa "Amazon", wimbo aliokiri kumtungia mkewe.
Mwaka huo hakutulia lengo lake la kupambana na vigogo wa muziki nchini Zaire haikuwa imekamilika.
Alijiunga na kundi lingine la "Yoka Lokole", kabla yake kuunda kundi lake sasa la "Viva La Musica" mapema mwaka wa 1977.
Vibao vyake ni kama Mwasi,Show me the way, Yolele, Mama,Proclamation"Chouchouna" (Papa Wemba), "Eluzam" na " Mbeya Mbeya" (Evoloko Lay Lay), "BP ya Munu" (Efonge Gina), "Mwana Wabi" , "Mizou" (Bimi Ombale) , "Zania" (Mavuela Somo. ,Emotion,Wake Up, Wake Up,Maria Valencia, Le Voyageur,Rail On, Kaokokokorobo ,Legend
Jela
Papa Wemba aliwahi kukamatwa kwa madai ya ulanguzi wa binadamu.
Tarehe 18 mwezi Februari 2003 maafisa wa idara ya upelelezi nchini Ufaransa walimkamata Papa Wemba kwa tuhuma za kuwaingiza raia wa Zaire (kama ilivyoitwa wakati huo DRC) barani ulaya kinyume cha sheria.
Image captionPapa Wemba
Mahakama ya ubelgiji ilimpata na hatia mwezi Juni mwaka wa 2003 na ikamhukumu kifungo cha mwaka mmoja na miezi mitatu jela.
Aidha mahakama hiyo ya Brussels ilimpiga faini ya euro 22,000.
Hata hivyo alitumikia kifungo cha miezi mitatu u nusu gerezani baada ya mdhamini kulipia dhamana ya Euro €30,000.
Alipoachiwa huru aliwaambia mashabiki wake kuwa aliyokumbana nayo akiwa gerezani yamemfunza mengi tu.
Katika utunzi wa wimbo wake "Numéro d'écrou" (2003)Papa Wemba anasimulia kukutana na mwenyezi Mungu akiwa gerezani.
Aidha anasema kuwa alibadilishwa mawazo na dini akitumikia kifungo.

No comments:

Post a Comment