Saturday, 14 May 2016

CUF WATANGAZA KUFUNGUA KESI DHIDI YA DR SHEIN

Mwanyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jeche

Chama Kinachoaminika kuwa kilishinda Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka jana, Chama cha Wananchi (CUF) jana, kimetangaza rasmi kuwa kimefungua kesi dhidi ya anayejiita Rais wa Zanzibar, katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC ), The Hague.

Kwa Mujibu wa Nassor Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, amesema kwamba, CUF kimefungua kesi hiyo dhidi ya rais wa Zanzibar, pamoja na viongozi wengine kwa madai ya kudhoofisha haki za kidemokrasia visiwani Zanzibar.

Mazrui amesema kwamba, kwa sasa CUF inasubiri maelekezo zaidi kutoka ICC juu ya kuanza na uendeshwaji wa kesi hiyo. Cuf inao ushahidi wa kutosha wa ushindi wa uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana.

Endapo ICC, itaridhia madai ya kesi ya CUF, itakuwa ni kesi ya kwanza ya Zanzibar, kufunguliwa na chama cha siasa katika mahakama hiyo tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania, mwaka 1992.

Mwanyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jeche alifuta matokeo ya uchaguzi wote Oktoba 28, 2015 kwa madai kuwa taratibu, kanuni na sheria zilikiukwa.

Hatua hiyo ya Jecha, kufuta uchaguzi huo ni baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuelekea kushinda katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka uliyopita.

Aidha, Mazrui amesema katika kesi hiyo, mbali na Rais wa Zanzibar, watu wangine waliyoshitakiwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa SMZ, na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

No comments:

Post a Comment