Saturday, 14 May 2016

MKUU WA WILAYA YA KINONDONI ANASA SHEHENA YA VIROBA

DC HAPI (3)
DC HAPI (3)
 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Ally Hapi Salum akikagua shehena ya pombe kali za viroba.
DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Ally Hapi Salum, amekamata shehena ya pombe kali za viroba, nyingine zikiwa zimekwisha muda wake wa matumizi.

Tukio hilo lilijiri kwenye ghala la mfanyabiashara mmoja maarufu (jina linahifadhiwa) jijini Dar es Salaam, Jumatano ya wiki hii wakati mkuu huyo wa wilaya akiwa katika msako wa kuwakamata wafanyabiashara  wanaodaiwa kuficha sukari, kutekeleza agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli.
DC HAPI (2)
Mkuu huyo wa wilaya alipofika maeneo ya barabara ya kwenda Mabibo, akiwa ameambatana na wasaidizi wake, ndipo alipoikuta shehena hiyo ya viroba ikiwa imehifadhiwa ghalani humo.
Ukiachilia mbali baadhi ya viroba hivyo kukutwa vimeisha muda wake wa matumizi, pia uhifadhi wake ulikuwa kinyume na utaratibu ambapo pembeni yake kulikuwa na maboksi mengi ya sabuni za unga za kufulia sambamba na vyakula, jambo ambalo ni hatari kiafya kwa watumiaji.
DC HAPI (4)
Mpaka gazeti hili linaondoka eneo hilo, polisi walikuwa wamelizingira ghala hilo pamoja na mmiliki wake kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Katika msako huo, mkuu huyo wa wilaya na jopo lake, walifanikiwa pia kukamata tani 27 za sukari zilizokuwa zimefichwa maeneo kadhaa, yakiwemo maghala bubu eneo la Manzese.
DC HAPI (5)
Hivi karibuni, Rais Magufuli akiwa mkoani Arusha aliagiza wafanyabiashara wote wanaoficha sukari na kusababisha iadimike mitaani, wakamatwe na sukari watakayokutwa nayo, igawiwe bure kwa wananchi jambo ambalo mpaka sasa limesababisha wafanyabiashara wengi nchini kupitiwa na rungu hilo.
Katika hatua nyingine, serikali kupitia mamlaka zinazohusika, hivi karibuni ilipiga marufuku uuzwaji wa viroba kwa madai kwamba vinachangia kwa kiasi kikubwa kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa kuwaathiri kiafya watumiaji wake ambao wengi ni vijana na kuchochea pia ajali za barabarani kutokana na madereva wengi wa magari na bodaboda kuvitumia wakati wa kazi.

No comments:

Post a Comment