Wednesday, 25 May 2016

Madaktari Tanzania wafanya upasuaji wa kihistoria

Upasuaji
Image captionMadaktari wamewafanyia upasuaji wagonjwa wawili
Madaktari wa Tanzania katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, wakishirikiana na wenzao wa India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo wa aina yake Tanzania.
Upasuaji huo ujulikanao kama ‘bypass surgery’ ulishirikisha kupandikizwa kwa mishipa ya damu kutoka sehemu nyingine ya mwili moyoni bila kutumia mashine ya kusimamisha moyo na mapafu.
Kwa kawaida madaktari wanasema upasuaji wa moyo hufanyika baada ya moyo na mapafu kusimama, lakini upasuaji huo ulifanyika wakati moyo na mapafu vikifanya kazi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa Bashir Nyangasa ameambia BBC kuwa upasuaji huo wa kupandikiza mishipa ya damu nje ya mshine ni wa kihistoria nchini Tanzania.
“Mgonjwa anaweza kutolewa mishipa ya damu kutoka miguuni au mikononi baada ya kupewa dawa ya usingizi na mishipa hiyo kupandikizwa kwenye mshipa wa moyo uliokuwa umeziba ili kuruhusu mzunguko wa damu wa moyo kama kawaida bila kutumia mashine,” amesema.
Upasuaji huo wa moyo kwa njia ya kupandikiza umefanyika kwa watu wawili, ambao umeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri .
Dkt Nyangasa amesema kwa sasa hakuna haja ya Watanzania wenye matatizo ya moyo kwenda nje ya nchi kwa kuwa wao kama wataalam wameweza kufanya upasuaji huo.
Anasema madaktari sasa wanaweza kuhudumia wagonjwa wengi zaidi wenye uhitaji na kupunguza gharama kwa serikali ya kusafirisha wagonjwa wa moyo nje ya nchi.
Mwandishi wa BBC aliyepo Dar es Salaam Esther Namuhisa anasema wengi wa wagonjwa wamekuwa wakisafiri hadi India ambapo wengi hukumbana na changamoto nyingi kupata huduma hiyo kifedha na hata kwenye upande wa lugha.

No comments:

Post a Comment