Saturday, 28 May 2016

TCRA yaiadhibu EATV kutokana na kucheza video ya wimbo ‘Panya’ wa Bracket, nayo E-FM yapata adhabu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekiadhibu kituo cha runinga cha East Africa Television (EATV) kulipa faini ya Tsh 3 milioni kutokana na kukiuka kanuni za utangazaji baada ya kuicheza video ya wimbo ‘Panya’ wa Bracket ambayo inadaiwa haina maadili ya kitanzania.
hh
Aidha, E-FM wameadhibiwa kulipa TSh 4 milioni baada ya kurusha kipindi cha Ubaoni kilichotoa simulizi ya msichana mchawi aliyekiri kuua.
Akisoma nakala ya hukumu hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini hapa jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda alisema baada ya kupitia maelezo ya utetezi kutoka kwa viongozi wa vituo hivyo, kamati hiyo imeamua kuitoza EATV faini ya Sh3 milioni na Sh4 milioni kwa E-Fm.
“Pamoja na adhabu hiyo tumetoa onyo kali kwa kukiuka kanuni ya maudhui, lakini pia endapo kosa hili litajirudia tunaahidi kutoa adhabu kali zaidi,” alisema.
Katika maelezo ya awali ya hukumu hiyo, Mapunda alisema adhabu ya EATV imetolewa baada ya kituo hicho kupitia kipindi chake cha ‘Muziki Mnene’ kurusha video ya wimbo wa Panya wa kundi la muziki la Bracket kutoka nchini Nigeria uliomshirikisha msanii Techno.
“Baadhi ya mavazi yaliyotumika katika wimbo huo hayaendani na maadili ya Kitanzania. Na kwa upande wa E-FM wameadhibiwa baada ya kurusha kipindi cha Ubaoni kilichotoa simulizi ya msichana mchawi aliyekiri kuua,” alisema Mapunda.
Baada ya kupokea nakala ya hukumu hiyo, Mkurugenzi wa EATV, Regina Mengi alisema hawana tatizo na adhabu hiyo na kwamba, atalifikisha suala hilo kwa uongozi wa kampuni yao.
“Bado siwezi kujibu lolote, uamuzi wa kuikubali au kukata rufaa itategemea na uamuzi wa bodi,” alisema.
Mkurugenzi wa E-FM, Scolastica Mazula alisema ameridhishwa na hukumu iliyotolewa, hivyo haoni kama kuna sababu ya kukata rufaa.
Mamlaka hiyo imevitaka vyombo vyote vya utangazaji nchini kuzingatia maadili na taratibu za sheria zinapofanya kazi ili kuepuka kuleta athari katika jamii.

No comments:

Post a Comment