Monday, 9 May 2016

Vigogo Chadema Kyela Wavuliwa Uongozi kwa Usaliti


Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Saadati Mwambungu
pamoja na wajumbe 19 wa kamati ya utendaji wa wilaya hiyo,
 wamevuliwa uongozi baada ya kutuhumiwa kukihujumu chama.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi jioni na uongozi wa Chadema
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, chini ya mwenyekiti wake,
 Dk Stephen Kimondo na Mratibu wa Kanda, Frank Mwaisumbe
 na kuweka wilaya hiyo chini ya uangalizi wa uongozi wa
 Mkoa wa Mbeya ndani ya siku 30 wakati wakiendelea na uchunguzi.
Mratibu wa Chadema katika Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe
 alisema jana kuwa baada ya kufanyia kazi tuhuma 17
 zilizowasilishwa kwao na wanachama wa chama hicho wilaya,
walibaini kuwa tuhuma saba kati yake zina ukweli dhidi ya viongozi
 hao hivyo wakafikia uamuzi wa kuwasimamisha na kuwataka
 kurudisha mali zote za chama hicho ndani ya siku 30.
“Ni kweli jana (juzi) tulifika Kyela na katika kikao chetu na kamati
 ya utendaji ya wilaya tulipowahoji ilionekana tuhuma saba zina ukweli
na baadhi ya watuhumiwa walikiri. Miongoni mwa tuhuma hizo ni
 matumizi mabaya ya fedha na mali za chama, kutoshiriki vyema
 Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hadi tukapoteza jimbo, hususani
siku ya kuhesabu kura za jumla viongozi walikimbia.
“Siku ile ya uchaguzi wa mwaka jana kuna vijana wetu walikamatwa
 wakituhumiwa kuvunja ofisi pale halmashauri ya Kyela na
 wakahukumiwa, lakini hakuna kiongozi yeyote ngazi ya wilaya
 aliyethubutu hata kwenda kuwaona pale gerezani hadi
 walipojinasua wenyewe,” alisema Mwaisumbe.
Alisema kutokana na mkutano wao wa juzi wajumbe wake
 kutotimia ili kufikia uamuzi halali wa kuwachukulia hatua zaidi,
 uongozi wa Kanda uliamua kuwasimamisha na chama kuwa
chini ya mkoa, huku ukifanyika utaratibu wa kuitisha mkutano
 mkuu ambao utawajadili kwa kina na kuona kama watafukuzwa
 moja kwa moja au la.
Mwambungu alipoulizwa juu ya kutimuliwa kwao, alikiri huku
akisisitiza kwamba tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote
kikatiba, na badala yake zimetengenezwa na ‘genge’ la watu
 wachache kwa uchu wa madaraka, lakini hana kinyongo
 kusimamishwa uongozi kwa kuwa ipo kikatiba ndani ya Chadema.
Alisema; “Kwanza ni heshima kwa kuwa jambo hili lipo kikatiba.
Lakini katika mkutano wa juzi akidi ya wajumbe haikutimia kwani
 Chadema Wilaya ya Kyela ina wajumbe 349 wa mkutano mkuu,
 lakini kwa juzi wajumbe waliohudhuria walikuwa 120 tu.
“Ndiyo maana uongozi wa Kanda ulitoa siku 30 za kufanyika
mkutano mkuu utakaowajumuisha wajumbe wote 349 na
 ndipo itakapofahamika… kama ni kufukuzwa au kuendelea na
 uongozi,”alisema.
Mwambungu alisema kati ya wajumbe 19 wa kamati ya utendaji
 ya wilaya, wajumbe saba waliamua kujiuzulu uongozi na baadaye
 wakaungana na wengine ambao waliunda tuhuma hizo kwa lengo
na kuuangusha uongozi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment